Mapishi ya futari za Ramadhani hayakamiliki bila kupika vibibi, shurba ya nyama ya mbuzi, mkate wa mofa, bokoboko la kuku na mihogo.
Mkate wa Mofa (Yemen)
Vipimo
Unga wa mahindi 1 mug
Unga wa mtama 2 mugs
Kitunguu maji 1 Kikubwa
Chumvi 1 Kijiko cha chai (Kidogo)
Sukari 1 Kijiko cha chakula
Hamira 1 Kijiko cha chai
Maji 3 mugs
Namna ya Kutayarisha na Kupika
- Upike unga wa mahindi kama uji kwa dakika kama tano na maji mug mbili.
- Uache upoe tia unga wa mtama na vitu vyote vilivyobaki pamoja na ile mug moja ya maji iliyobaki.
- Uache mpaka uumuke.
- Fanya maduara duara halafu tandaza uchome kwa moto mdogo kama chapati bila ya mafuta kwenye kikaango (frying pan). Choma mmoja mmoja yote hadi umalize..
- Lipange kwenye sahani tayari kwa kuliwa na mchuzi wa nazi wa samaki au kuku au vyovyote upendavyo.
Muhogo, Samaki wa Kuchoma na Bamia
Vipimo
Mihogo (fresh) 3 - 4
Tui la kopo au (box) 1000 ml
Chumvi 1 kijiko cha chai
Kitunguu maji kilokatwakatwa 1
Nyanya mshumaa/tungule) 3-4
Pilipili mbichi ndefu 2-3
Pilipili boga 2
Namna ya Kutayrisha na Kupika
- Menya mihogo kisha ikate kate vipande inchi tatu hadi nne, kila kipande kigawe kitoke vipanda vinne. Toa mzizi katikati.
- Osha mihogo ipange kwenye sufuria ya nafasi na yenye mfuniko, ili upate nafasi ya kutia viungo unavyoona pichani na utokotaji wa tui wahitaji nafasi.
- Panga/tandaza kitunguu, nyanya mshumaa/tungule, pilipili mbichi na pilipili boga juu ya mihogo, tia chumvi na tui lote.
- Funika sufuria kisha weka jikoni moto wa kiasi kuchemsha tui lipande juu. Hakikisha tui halifuriki na kumwagika kwa kuchungulia au kufunika nusu mfuniko
- Kwa muda wa nusu saa hivi ukiona sasa tui linatokota chini chini funika mfuniko na upunguze moto mdogo kabisa tui likauke kidogo na liwe zito.
- Toa muhogo mmoja ubonyeze ukiona umeiva zima jiko na wacha sufuria hapo kwa muda wa dakika 10. Mihogo iko tayari kuliwa.
Kidokezo
Tui lote huwa chini baada ya mihogo kuiva unapopakuwa teka kutoka chini uweze kupata uzito wa tui umwagie juu.
Bamia/Mabenda
Vipimo
Bamia Robo kilo
Nyanya/Tungule 3
Kitunguu maji 1
Thomu ya unga au ilosagwa 1 Kijiko cha chai
Nyanya kopo (tomato paste) 1 Kijiko cha supu
Mafuta 150 ml
Chumvi 1 Kijiko cha chai
Pilipili boga 1
Namna ya Kutayarisha na Kupika
- Kata vichwa vya bamia kisha zikate kate mara mbili zikiwa kubwa, ikiwa ni ndogo mno haina lazima kuzikata osha tu uweke kando.
- Katika sufuria, katakata kitunguu, nyanya, pilipili boga tia ndani viungo hivi ongeza chumvi, mafuta, thomu na nyanya kopo
- Washa moto mdogo mdogo huku umefunika sufuria kwa muda wa dakika 20 kisha ukiona mboga zimeshika kutokota ongeza bamia koroga.
- Tia maji 200ml (glasi 2) wacha kwa muda wa dakika 15 kupikika tena, ukionja utamu wa mboga na chumvi, hakikisha bamia pia zimeiva. Hapa Bamia zipo tayari kuliwa.
Samaki wa Kuchoma
Vipimo
Samaki (dorado) au mikizi au tuna 2 Wakubwa (fresh)
Chumvi 1 Kijiko cha chai
Thomu ya unga au iliyosagwa 1 ½ cha chai
Tangawizi mbichi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu
Namna ya Kutayrisha na Kuchoma
- Safisha samaki vizuri mchane chane (slit) kwa ajili ya kuweka masala.
- Changanya viungo vyote na chumvi, kisha paka katika samaki nje na ndani na sehemu ulizochanachana. Mloweke kwa muda wa robo saa hivi.
- Weka karatasi ya jalbosi (foil paper) katika tray (treya) ya oveni. Muweke samaki kisha mpike (grill) kwa moto wa juu achomeke hadi samaki agueke rangi na aive.
Kidokezo
Kuweka karatasi ya jalbosi katika tray ya oveni kunasaidia kuhifadhi tray kuchafuka na tabu ya kusugua na kuiosha.
Hariys - Bokoboko la Kuku
Vipimo
Ngano nzima (shayiri) 3 Vikombe
Kuku ½ (3 lb au kilo moja na nusu)
Thomu na tangawizi iliyosagwa 1 Kijko cha supu
Pilipili manga ya unga ½ Kijiko cha chai
Jiyrah (cumin/bizari ya pilau) ½ Kijiko cha chai
Chumvi Kiasi
Kidonge cha supu (Curry cube) 1
Samli ya moto ½ Kikombe
Namna ya Kutayarisha na Kupika
- Loweka ngano (shayiri) tokea usiku au muda wa masaa.
- Katakata kuku mtie katika sufuria, tia maji kiasi na viungo vyote. Mchemeshe aive na ibakie supu yake.
- Toa kuku, toa mifupa na umchambue chambue vipande vidogo vidogo.
- Chemsha ngano (shayiri) kwa kufunika sufuria hadi iive na kukauka maji.
- Tia supu ya kuku katika ngano (shayiri), na kuku uliyemchambua. Tia kidonge cha supu (curry cube)
- Tia samli nusu (bakisha nusu) kisha changanya mchanganyiko hadi uvurugike kuku na ngano (shayiri) vizuri.
- Mimina katika sahani, mwagia samli ya moto iliyobakia ikiwa tayari.
Kidokezo
Ukipenda kulia na sukari
Shurba ya Nyama ya Mbuzi
Vipimo
Nyama ya mbuzi 2lb (Kilo moja)
Nyanya 1
Kitunguu maji 1
Kidonge cha supu (curry cube) 1
Maji 4 Mugs
Thomu 1 Kijiko cha supu
Bizari ya pilau (cumin) 1 Kijiko cha chai
Bizari ya manjano ½ Kijiko cha chai
Mdalasini 1 Kijiti
Shairi (oats) 5 Vijiko supu
Pilipili mbichi 2
Siki ya zabibu (Grape vinegar) 2 Vijiko vya supu
Chumvi Kiasi
Namna ya Kutayarisha na Kupika
- Osha nyama vizuri tia kwenye sufuria.
- Katakata kitunguu na nyanya, ikiwa hupendi maganda ya nyanya toa na ukate kate.
- Tia kidonge cha supu, mdalasini, chumvi na maji funika uchemshe nyama mpaka iive.
- Tia shairi (oats) kwenye bakuli na maji iache, nusu saa kisha isage kidogo tu, na mimina kwenye supu ya nyama.
- Tia pilipili mbichi nzima, thomu, bizari zote na siki. Weka moto mdogo mdogo huku unakoroga kila baada ya muda.
- Tazama uzito, na ongeza maji kidogo ikiwa nzito sana
Kidokezo
Ikiwa huna siki ya zabibu tia ndimu au limao au white vinegar.
Vibibi
Vipimo
Mchele 2 Vikombe
Tui la nazi 1 1/2 Kikombe
Mafuta 1 Kijiko cha supu
Hamira 2 Vijiko vya chai
Unga wa ngano 1 Kijiko cha supu
Hiliki Kiasi upendavyo
Sukari ¾ au 1 Kikombe
Namna ya Kupika na Kutayarisha
- Osha na loweka mchele usiku mzima ndani ya maji baridi.
- Mimina vifaa vyote isipokuwa sukari , ndani ya mashine ya kusagia (blender) na usage mpaka mchele uwe laini.
- Mimina ndani ya bakuli na ufunike , kisha weka pahali penye joto ili mchanganyiko ufure/uvimbe.
- Ukishafura , mimina sukari na changanya vizuri ; ukiona mchanganyiko ni mzito sana, ongeza maziwa kidogo.
- Weka chuma kipate moto.
- Paka mafuta au samli kidogo kwenye chuma kisha mimina mchanganyiko kiasi kuunda duara na ufunike.
- Utazame ikishaiva upande mmoja , geuza upande wa pili mpaka iwe tayari.
- Endelea Mpaka umalize mchanganyiko wote; panga kwenye sahani na tayari kuliwa.
Kidokezo
Unaweza kutumia chuma kisichoganda ( non stick ); nacho hakitaraji kutiwa mafuta.
Vibibi vya Tui la Nazi
Vipimo
Mchele 2 Vikombe
Tui la nazi zito 2 Vikombe
Hamira 1 Kijiko Cha chai
Unga wa ngano 2 Vijiko vya supu
Iliki Kiasi upendavyo
Sukari Kiasi upendavyo
Yai 1
Vipimo vya Tui la Kupaka
Tui la nazi 2 Vikombe
Hiliki ya unga Kiasi upendacho
Sukari Kiasi upendacho
Unga wa ngano 1 Kijiko cha supu
Namna ya Kutayarisha na Kupika
- Changanya vitu vyote vya tui la kupaka katika kisufuria kidogo.
- Lipike tui huku walikoroga mpaka lichemke na liwe zito.
- Osha na loweka mchele usiku mzima ndani ya maji baridi.
- Mimina vifaa vyote isipokuwa yai na sukari , ndani ya mashine ya kusagia (blender) na usage mpaka mchele uwe laini.
- Mimina sukari na yai usage kidogo tu kiasi cha kuchanganya.
- Mimina ndani ya bakuli na ufinike , kisha weka pahali penye joto ili mchanganyiko ufure/uvimbe
- Ukishafura, weka chuma kipate moto. (Ni bora kutumia kichuma kidogo)
- Katika sahani ya kupakulia, paka tui kote.
- Tia kijiko nusu cha chai cha mafuta au samli kwenye chuma kisha mimina mchanganyiko ukitumia upawa na ufunike.
- Kibibi kikianza kuiva na kushikana upande mmoja , kigeuze upande wa pili mpaka kigeuke rangi na kuiva.
- Panga kwenye sahani iliyopakwa tui.
- Endelea Mpaka umalize mchanganyiko wote; kila ukiepua kibibi, panga juu ya mwenzake kama ilivyo kwenye picha na upake tui juu yake.
Usikose makala zifuatazo za mahanjumati ya Eid.
Shukrani kwa tovuti ya www.alhidaaya.com kwa makala hii.