Print this page
Mapishi ya Futari
Mapishi

Mapishi ya Futari

Ni kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ni kipindi cha mfungo kwa ndugu Waislam kote duniani. Kwa kulitambua hilo, wavuti yako ya TanzMED itakuwa ikikuletea makala mbalimbali kuhusu mapishi ya aina mbalimbali ya futari za mwezi huu wa Ramadhani. Vyakula hivi pia vinaweza kupikwa hata na wale ambao hawako kwenye mfungo wa mwezi wa Ramadhani, kwa wakristo wakati wa kwaresma au siku yoyote ile.

Pilau ya Sosi ya Soya na Mboga

 

 

 

 

 

Vipimo

Kuku (mkate vipande vipande) 1

Mchele wa Basmati (lowanisha) 3 magi (1 mug)

Mdalasini 1 mche mmoja

Vitunguu maji (vilivyokatwa vyembamba) 6

Mchanganyiko wa mboga za barafu 1 magi (1 mug)

(karoti, mahindi, njegere)

Kabichi (iliyokatwa katwa nyembamba) 1 magi (1 mug)

Pilipili mbichi (iliyosagwa) 3

Pilipili boga iliyokatwa vipande vidogo vidogo 1

Pilipili manga 1 kijiko cha chakula

Chumvi 1 kijiko cha chakula

Sosi ya soya (soy sauce) 5 vijiko vya chakula

Kotmiri iliyokatwa katwa 1 magi (1 mug)

Thomu na tangawizi iliyosagwa 2 vijiko vya chakula

Namna ya Kutayarisha na Kupika

  • Tia mafuta ndani ya karai. Yakipata moto kiasi, mimina vitunguu maji na mdalasini 1 mzima kaanga. Itachukua muda kidogo. Kaanga mpaka viive viwe rangi ya hudhurungi (brown). Viepue na uweke kando.
  • Ndani ya sufuria kubwa, mimina kuku, chumvi, thomu (kitunguu thomu) na tangawizi, sosi ya soya, pilipili manga, pilipili mbichi, chemsha mpaka kuku aive na maji yakauke.
  • Changanya vitunguu ulivyokaanga, kabichi, pilipili, mboga, kotmiri, mchanganyiko wa mboga za barafu na weka kwa muda wa dakika tano au kumi. Tia na mafuta kidogo uliyokaangia vitunguu .
  • Chemsha mchele na chumvi uive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja (wali wa maji). Ukishauchuja umwagie katika masala ya kuku.
  • Nyunyizia mafuta kidogo uliokaangia vitunguu.
  • Weka moto mdogo mpaka wali ukishaiva, uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa.

Dokezo

Unaweza kuupika wali huo ndani ya jiko, yaani badala ya kutia masala kwenye sufuria ukayatia katika bakuli au treya (tray) ya jiko (oven), kisha ukamwagia wali uliouchuja humo na kuupika katika moto wa nyuzi joto 400-450 kwa muda wa dakika 15-20.

Kabaabu za Kuchoma katika Vijiti

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Nyama ya kusaga 3 lb (au kilo moja na nusu)

Thomu 1 kijiko cha chakula

Tangawizi 1 kijiko cha chakula

Chumvi Kiasi

Kotmiri 1 msongo

Bizari ya kababu ½ pakiti ya 100g

(Shan Chapplin Kabaab mix)

Namna ya Kutayarisha na Kupika

  • Saga nyama pamoja na kotmiri mara mbili iwe laini kuliko ya sambusa.
  • Tia kwenye bakuli na changanya na vitu vyote pamoja.
  • Viringisha kwenye vijiti vya kuchomea na acha kama muda wa saa.
  • Choma (bake) katika oven kwa moto wa 350?c mpaka zigeuke rangi na kuiva.
  • Zikishaiva ziweke kwenye sahani tayari kwa kuliwa na saladi, chips, mikate au wali.

Dokezo

  • Ni vema kuloweka vijiti vya kuchomea kwenye maji usiku nzima ili ukichoma kababu vijiti visiungue.
  • Tumia bizari zako mwenyewe upendazo ikiwa huna hiyo ya Shan Chapplin Kabaab Mix.

Sharbati ya Maziwa na Shira ya Rozi

 

 

 

 

 

 

 

Vipimo

Shirah ya Rozi (rose syrup) ½ kikombe cha chai

Vipande vya barafu 1 Kikombe cha chai

Maziwa 4 Kikombe cha chai

Namna ya Kutayarisha

  • Tia maziwa, shirah ya rozi na barafu katika jagi la kusagia (blender)
  • Saga kwa muda wa dakika moja au mbili.
  • Mimina sharbati kwenye gilasi ikiwa tayari.

Shukrani za Kipekee kwa tovuti ya http://www.alhidaaya.com kwa kututumia makala hii.

Kwa niaba ya timu nzima ya Tanzmed tunawatakia mfungo mwema wa mwezi wa Ramadhani. Ramadhan kareem..

Imehaririwa Jumanne, 09 Juni 2020 11:50
Tagged under
Share
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Makala zaidi kutoka kwa Dr Khamis

Makala shabihana